Kwanini Wanaume Wengi Wanakufa Mapema?

By | June 21, 2018

Kifo ni hatua ya mwisho ya kiumbe hai. Binadamu baada ya kupitia hatua mbalimbali za ukuaji tangu akiwa tumboni kwa mama na baadaye kuzaliwa na kuendelea na ukuaji huo kupitia hatua kuu nne ambazo ni utoto, ujana, utu uzima na uzee na mwishowe hufa.

Hata hivyo si binadamu wote wanaofika katika hatua ya uzee wengi hufariki kabla ya kufikia hatua hiyo. Kuna sababu mbalimbali zinazopelekea kifo kabla ya uzee. Kubwa zaidi ukweli ni kwamba mara nyingi wanaume hufariki mapema kuliko Wanawake. Ni wazi kabisa katika jamii nyingi wazee wa kiume huwa kidogo sana kwa idadi ukilinganisha na idadi ya wazee wa kike. Inakadiriwa kuwa mwanamke anaishi miaka 5 hadi 10 zaidi ya mwanaume.

Makala hii itazungumzia sababu zinazopelekea wanaume kufariki katika umri mdogo kuliko wanawake.

(a) Sababu za kiafya
i. Kupotea kwa kromosome Y: Katika hatua ya utu uzima mwanaume hupoteza kromosome Y katika seli nyekundu za damu. Kupotea kwa kromosome Y humuweka mwanaume katika hatari zaidi ya kupata magonjwa ya kansa na Mfumo wa fahamu ambayo mara nyingi hupelekea kifo.

ii. Wanaume wanatazamiwa kufa kwa Magonjwa ya moyo kuliko wanawake. Ni ukweli ulio wazi kuwa wanaume wengi (50%) wanasumbuliwa na magonjwa ya moyo katika hatua yao ya ujana kuliko wanawake. Sababu kuu inadhaniwa kuwa ni uchache wa kiwango cha homoni ya estrojeni ambayo ina uwezo wa kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo. Wanawake wana kiwango kikubwa cha homoni hii na hivyo kuwapunguzia hatari ya kupata magonjwa ya moyo.

iii. Kujitenga na Jamii: Kwa sababu za kisaikolojia ambazo hadi sasa hazijapatiwa ufumbuzi inasemekana kuwa wanaume wengi wanaopenda kujitenga na jamii na kuishi katika upweke peke yao hufariki mapema.

iv. Wanaume wengi hawapati huduma za afya: Utafiti uliofanywa na Chuo cha Utibabu Harvard (Marekani) umebaini kuwa wanaume wengi hawana utaratibu wa kumwona daktari wanapopatwa na matatizo ya kiafya, hivyo hii nayo inaweza kuwa sababu inayopelekea wanume kufariki mapema kuliko wanawake.

(b) Sababu nyingine
i. Wanaume wengi hujihusisha katika kazi hatarishi: Miongoni mwa sababu zinazopelekea wanaumea wengi kufa katika umri mdogo ukilinganisha na wanawake ni kwamba wanaume wengi wanajihusisha katika kazi ambazo zinawaweka katika hatari ya kifo kama vile Vita, Kuendesha mitambo viwandani, Ujambazi n.k.

ii. Wanaume wengi hujinyonga; Kutokana na matatizo na misukosuko mbalimbali inayowakabili binadamu hususani vijana, Ni wazi kuwa wanaume wengi hushindwa kuvumilia misukosuko hiyo na kuamua kujinyonga. Migogoro ya kimapenzi inadaiwa kuwa ndio chanzo kikubwa ya vijana wanaume kujinyonga, Sababu nyingine ni madeni, aibu, hofu ya kifungo na Ufukara.

Nini kifanyike ili kuwasaidia wanaume?
Jambo kubwa na la msingi linaloweza kufanyika ili kuokoa maisha ya wanaumea ni kuchukua tahadhari ya kiafya katika kila sababu zilizoainishwa hapo juu kama vile
i. Wanaume wawaone madaktari kwa ushauri na matibabu wanapopata matatizo ya kiafya
ii. Wanaume wanatakiwa waombe ushauri wanapokutwa na matatizo ya kijamii na sio kuchukua hatua ngumu ya kujinyonga.
iii. Wanaume waache kuvuta sigara kwani huongeza kasi ya kansa na magonjwa ya moyo.
Hii haimaanishi wanawake waende kinyume na wanaume lahasha, bali nao wajitahidi kuchukua hatua/ tahadhari za kiusalama na jinsi ya kuyaepuka matatizo na magonjwa hatarishi yanayopelekea kifo.

One thought on “Kwanini Wanaume Wengi Wanakufa Mapema?

  1. Jacob Mushi

    Habari Rafiki, Leo ni siku nyingine tena ambayo tumepewa kama zawadi kwa ajili ya kwenda kuyafanya Maisha yetu yawe bora Zaidi.

    Jisemeshe Maneno Haya Kabla Hujatoka Kwenda kufanya Chochote.

    “NACHUKUA HATUA, NAJIFUNZA, NAWEKA JUHUDI NA BIDII, NAVUMILIA.
    MAFANIKIO NI HAKI YANGU, EEH MUNGU NIWEZESHE.”

Leave a Reply